Afariki Baada ya Kuona Maiti za Ajali ya Ndege

Sunday, May 16, 2010 / Posted by ishak /


Afisa mmoja wa Libya amefariki baada ya kuona maiti za ajali ya ndege wakati alipokimbilia kwenye eneo la tukio kutoa msaada.
Afisa huyo ambaye ni mlinzi kwenye uwanja wa ndege alifariki baada ya kuona maiti za watu 102 waliokuwemo kwenye ndege ya Libya ambayo ililipuka wakati wa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Tripoli.

Taarifa zinasema kuwa mlinzi huyo alikimbilia kwenye eneo la ajali kwa nia ya kutoa msaada lakini alipofika na kuziona maiti zikiwa zimezagaa kila kona ugonjwa wake wa kisukari ulimzidia na hapo hapo aliiaga dunia.

Taarifa zaidi kuhusiana na kifo chake hazikutolewa ingawa taarifa zilisema kuwa mlinzi huyo alikuwa ni mzee.

Wakati huo huo mtu pekee aliyenusurika kwenye ajali hiyo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, Ruben, amesafirishwa leo kurudishwa kwao Uholanzi.

Ruben alikuwa na baba yake, mama yake pamoja na kaka yake mwenye umri wa miaka 11 kwenye ndege hiyo lakini wote walifariki kwenye ajali hiyo.

Ruben na wazazi wake pamoja na kaka yake walikuwa likizo nchini Afrika Kusini kusherehekea ndoa ya wazazi wake kutimiza mwaka mmoja.

Shangazi na mjomba wake toka Uholanzi walikimbilia mjini Tripoli kuwa karibu na mtoto huyo ambaye alikuwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha kadhaa kwenye miguu yake.

Mtoto huyo ameishaambiwa na shangazi yake kuwa wazazi wake na kaka yake wamefariki kwenye ajali hiyo mbaya ya ndege

source nifahamishe