Waislamu Walazimishwa Kula Nguruwe Ili Ziwape Nguvu

Sunday, May 16, 2010 / Posted by ishak /


Wanawake watatu wa kiislamu toka nchini Indonesia walilazimishwa na bosi wao katika kiwanda cha nguo nchini Taiwan wale nyama ya nguruwe ili ziwape nguvu na stamina ya kufanya kazi.
Wanawake watatu wa kiislamu ambao ni raia wa Indonesia, walilazimishwa na bosi wao katika kiwanda cha nguo mjini Taipei wale nyama ya nguruwe au la mishahara yao itapunguzwa.

Kwa muda wa miezi saba wanawake hao walilazimishwa na bosi wao kula vyakula vyenye nyama ya nguruwe vilivyokuwa vikigaiwa kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho kwakuwa bosi wa kiwanda hicho alikuwa akiamini kuwa nyama ya nguruwe ingewapa nguvu na stamina ya kufanya kazi wanawake hao.

Bosi wa kiwanda cha nguo cha Shin Hua Hang Fashion Co, Chang Wen-lin amefikishwa mahakamani kwa kuwalazimisha wanawake hao wale nyama ya nguruwe katika kipindi cha ajira yao kuanzia mwezi septemba 2008 hadi April 2009.

Katika jalada la kesi aliyofunguliwa mahakamani, Cheng aliamini kuwa nyama ya
nguruwe ingewapa stamina ya kufanya kazi wanawake hao na alitishia kuwakata mishahara yao iwapo wasingekubali kula nyama hiyo.

Waendesha mashtaka wanataka Chang Wen-Lin ahukumiwe kwenda jela miezi minane.

Wanawake hao walipelekea malalamiko yao kwa taasisi ya kutetea wafanyakazi mjini Taipei ambapo walisema kuwa walifanyishwa kazi nyingi kuliko kawaida katika kipindi cha miezi minane bila ya kulipwa chochote.

Taasisi hiyo ndiyo ililifikisha suala hilo mahakamani kwa niaba ya wanawake hao ambao kutokana na hofu za masuala ya uhamiaji walikuwa wakihofia kurudishwa kwao iwapo wangemchukulia hatua bosi wao.

Wanawake hao hivi sasa wametafutiwa kazi kwenye kampuni nyingine mjini Taipei.

Kuna vibarua takribani 350,000 nchini Taiwan ambapo wengi wao wanatoka Indonesia, Philippines na Vietnam.

Katika ripoti ya mwaka 2009 ya haki za binadamu duniani, tatizo kubwa lililotajwa kuikabili Taiwan lilikuwa ni unyanyasaji wa wafanyakazi makazini.

Ripoti hiyo ilisema kuwa wafanyakazi wengi huogopa kuripoti matatizo yanayowakabili kwa kuhofia kupoteza ajira zao.

source nifahamishe