Aliyeiba Mtoto Toka Kwenye Mimba ya Mwenzake Afungwa Maisha

Tuesday, May 18, 2010 / Posted by ishak /


Mwanamke wa nchini Marekani ambaye alimlaghai mwanamke mjamzito na kumpeleka nyumbani kwake kabla ya kulipasua tumbo lake kwa kisu kwa nia ya kuiba kichanga chake, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mwanamke wa nchini Marekani ambaye alikuwa na shauku ya muda mrefu ya kuwa na mtoto, amehukumiwa kwenda jela maisha baada ya kuiba kichanga toka kwenye tumbo la mwanamke mjamzito.

Andrea Curry-Demus, 40, alipatikana na hatia ya kumuua mwanamke mjamzito Kia Johnson, 18 baada ya kulipasua tumbo lake na kisha kuiba kichanga kilichokuwa tumboni mwake na kujifanya yeye ndiye aliyejifungua kichanga hicho.

Curry-Demus akisomewa hukumu yake aliigeukia familia ya Kia na kuwaambia "Naomba mnisamehe".

"Naiomba radhi familia yake", alisema Curry-Demus kabla ya kumgeukia jaji na kusema "Nimekosa".

Mama yake Kia, Darlene Lee, aliridhishwa na hukumu iliyotolewa ya kifungo cha maisha jela akisema kuwa hakutaka Curry-Demus ahukumiwe adhabu ya kifo kwakuwa anataka ateseke kwa uovu alioufanya.

"Nataka ateseke na aione sura ya mwanangu kila siku anapoamka, afikirie kitendo alichofanya".

Hili si tukio la kwanza la Curry-Demus kujaribu kuiba kichanga toka kwenye tumbo la mwanamke mjamzito, miaka 20 iliyopita, Curry-Demus alihukumiwa kwenda jela miaka 10 baada ya kumchoma na kisu tumboni mwanamke mjamzito akiwa
na nia ya kulipasua tumbo lake na kuiba kichanga chake.

Katika tukio la hivi karibuni Curry-Demus aliiongopea familia yake kuwa yeye ni mjamzito baada ya kumlaghai Kia na kujifanya rafiki yake.

Alikuwa akitamba kwa marafiki zake kuwa yeye ni mjamzito akiwaonyesha picha ya Ultrasound aliyoiiba toka kwa Kia na kisha kuibandika jina lake.

Baada ya kutimiza azma yake ya kuiba kichanga cha Kia, aliiambia familia yake kuwa amejifungua mtoto kabla ya muda wake ingawa vipimo vya hospitali havikuonyesha kama aliwahi kuwa mjamzito.

Alitiwa mbaroni baada ya maiti ya Kia kugundulika nyumbani kwake baada ya majirani kulalamikia harufu kali toka nyumbani kwake.

Kichanga alichokiiba kilinusurika maisha yake na kiliwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment