Wanaume wawili wa nchini Malawi ambao waliiga tamaduni za watu wa magharibi na kuamua kuoana na kufanya sherehe kubwa, wamehukumiwa kwenda jela miaka 14 pamoja na kufanyishwa kazi ngumu.
Akitoa hukumu jaji wa mahakama ya Blantyre, Nyakwawa Usiwa-Usiwa alisema kuwa anatoa hukumu kali ili kuwalinda wananchi na watu wenye tabia kama ya wanaume hao waliooana.
Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walitupwa jela tangia walipotiwa mbaroni mwezi disemba mwaka jana wakati walipofanya sherehe ya harusi yao.
Kukamatwa kwa Monjeza na “mkewe” Tiwonge Chimbalanga kulisababisha Malawi iingie kwenye mgogoro mkubwa na mataifa ya magharibi ambayo yanatoa msaada kwa Malawi. Uingereza ambayo ndiyo mfadhili mkubwa wa Malawi iliweka wazi kukasirishwa kwake na kesi hiyo lakini haikusitisha misaada yake.
Mahakama ilijaa mamia ya watu na wengine walijaa nje ili kujua hukumu ya Monjeza na mwenzake. Walipotolewa mahakamani kupelekwa jela kuanza kutumikia vifungo vyao, baadhi ya watu walipiga kelele na kuwatupia maneno ya kejeli.
“Mmepata mlichostahili”, “Miaka 14 haitoshi ilibidi mfungwe jela miaka 50”.
Akiongea wakati wa kutoa hukumu, Jaji Usiwa-Usiwa alisema “Nitawapa hukumu ya kutisha ili kuilinda jamii na watu kama nyinyi na iwe mfano kwa wengine”.
Wakili wa washtakiwa aliitaka mahakama itoe adhabu ndogo kwakuwa vitendo vya Monjeza na mwenzake havimdhuru mtu mwingine yeyote.
“Ni watu wawili watu wazima ambao wanafanya mambo yao kwa siri. Hakuna mtu atakayedhurika iwapo wataruhusiwa kurudi kwenye jamii”, alisema wakili huyo.
Nayo taasisi ya kutetea haki za binadamu ya Cedep ya nchini Malawi, ilisema kuwa leo ni siku mbaya sana kwa Malawi.
“Inakuwaje wafungwe miaka 14 eti kwakuwa wanapendana? Hata kama wakifungwa jela miaka 20 jinsia zao haziwezi kubadilika”, mwanaharakati wa taasisi hiyo.
Jaji Usiwa-Usiwa alisema kuwa wanaume hao hawakuonyesha dalili yoyote ya kujutia tabia yao mbaya ya Sodoma na Gomora.
Wakati huo huo Marekani imelaani hukumu iliyotolewa na imesema kuwa hukumu hiyo ni hatua moja nyuma katika kulinda haki za binadamu.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment