Jela Mwaka Mmoja Kwa Kumpiga Chabo Mkewe Akioga

Thursday, March 11, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume wa nchini Marekani ambaye alitoboa tundu kwenye ukuta wa bafu lake na kuchukua video kwa siri wakati mkewe akioga amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja.
Richard Perez mkazi wa Minnesota nchini Marekani amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja kwa kurekodi video kwa siri wakati mkewe akioga.

Mahakama iliambiwa kuwa Perez alitoboa tundu kwenye ukuta wa bafu lake na kisha kutegesha video kamera ambayo aliitumia kurekodi video za siri wakati mkewe alipokuwa uchi akioga.

Mkewe ambaye alitajwa kwa kifupi kama KP, aliwaita polisi baada ya kukuta video zake akioga kwenye kompyuta iliyopo nyumbani kwao.

Wapenzi hao walikuwa kwenye taratibu za kuivunja ndoa yao wakati video hizo zilipogundulika.

Polisi walizikuta video nne za KP akivua nguo zake na kuingia kwenye bafu kuoga. Pia polisi walifanikiwa kuzipata video kadhaa zilizopigwa na Perez kwenye maeneo ya hadhara ambapo alichukua video za wanawake chini ya sketi zao.

Perez alipatikana na hatia januari mwaka jana kutokana na makosa ya kuchukua video ya mke wake akiwa mtupu akioga bila ya yeye mwenyewe kujua.

"Mke anaweza akawa na masuala binafsi anapokuwa peke yake bafuni na hiyo haimaanishi kuwa kwasababu ya ndoa haki zake za masuala binafsi ndio zipotee", alisema jaji wa kesi hiyo wakati akimhukumu Perez kwenda jela mwaka mmoja.

Perez alikata rufaa lakini juzi mahakama ilitupilia mbali rufaa yake kumuamuru aende jela akatumikie kifungo chake cha mwaka mmoja.


source nifahamishe