Sala ya Myahudi Yasababisha Kasheshe Kwenye Ndege

Thursday, January 21, 2010 / Posted by ishak /


Myahudi aliyeamua kusali ndani ya ndege nchini Marekani alizua hofu kwa abiria wengine kiasi cha kuifanya ndege itue kwa dharura.
Myahudi aliyeamua kutoa zana zake za kusalia ndani ya ndege ya Marekani na kuanza kusali kwa sauti, alisababisha hofu ya bomu na kupelekea ndege hiyo ibadili mwelekeo na kutua uwanja wa ndege wa karibu.

Myahudi huyo alikuwa kwenye ndege ya Chautauqua Airlines iliyokuwa ikitokea New York kuelekea Louisville, Kentucky.

Ndege hiyo ilibadili mwelekeo na kutua kwa dharura kwenye uwanja wa ndege wa Philadelphia International Airport baada ya Myahudi huyo kutoa viboksi viwili vyeusi na kujifunga mkononi na kichwani kabla ya kuanza kusali kwa sauti.

Katika sala za kiyahudi, viboksi viwili vidogo vyeusi vyenye mikanda hufungwa kichwani na mkononi kabla ya sala kuanza.

Abiria katika ndege hiyo ambao hawajawahi kuona sala za kiyahudi zinavyofanyika walidhania viboksi hivyo ni mabomu na myahudi huyo ndio alikuwa akijiandaa kujilipua.

"Alikuwa akisali kwa sauti huku akiwa amevaa viboksi vyake vyeusi, lugha aliyokuwa akiongea hakuna aliyekuwa akiielewa", alisema abiria mmoja.

Magari 12 ya polisi na timu ya wataalamu wa mabomu walikuwepo kwenye uwanja wa ndege wa Philadelphia wakati ndege hiyo ilipotua kwa dharura.

Myahudi huyo alikamatwa na kuhojiwa wakati wataalamu wa mabomu wakiisachi ndege nzima kuangalia kama kuna bomu lolote.

Myahudi huyo alichiwa huru baada ya kugundulika kuwa viboksi vyake vyeusi havikuwa mabomu bali ni vifaa vinavyotumiwa katika sala za kiyahudi.

Ulinzi katika masuala ya anga umeimarishwa zaidi nchini Marekani tangia disemba 25 mwaka jana baada ya kijana wa Kinigeria kufeli jaribio lake la kujipua kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Marekani.


source niffahamishe