Walinzi wa Kivita Kuzilinda Timu Zitakazoshiriki Kombe la Dunia

Wednesday, January 20, 2010 / Posted by ishak /


Baada ya basi la wachezaji wa Togo kushambuliwa kwa risasi nchini Angola wakati wakiwasili kwaajili ya kombe la mataifa ya Afrika, timu zitakazoshiriki kombe la dunia nchini Afrika Kusini baadae mwaka huu zinakusudia kukodisha walinzi wa kivita toka nchini Iraq na Afghanistan.
Timu nyingi zitakazoshiriki kombe la dunia baadae mwaka huu nchini Afrika Kusini zimepanga kuwakodisha walinzi toka makampuni ya ulinzi katika sehemu zenye vita za nchini Iraq na Afghanistan.

Walinzi hao wakiwa na silaha za kivita watawalinda wachezaji na maafisa wa timu zitakazoshiriki kombe la dunia.

Taarifa zilizopatikana zilisema kwamba baadhi ya vyama vya soka katika nchi za barani Ulaya na Kusini mwa Amerika tayari zimeishawakodisha walinzi wa kivita ili kuwalinda wachezaji wao na familia zao muda wote watakaokuwa nchini Afrika Kusini.

Walinzi hao wakitumia silaha za kivita, magari yasiyopitisha risasi watawalinda wachezaji masaa 24 na kuwaepusha na matukio ya utekaji.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia hofu ya usalama nchini Afrika Kusini ambapo matukio ya uhalifu yamekuwa yakitokea kwa kiwango kikubwa sana kila siku.

Hata hivyo shirikisho la soka duniani limezihakikishia usalama nchi zitakazoshiriki kombe la dunia kutokana na hatua ya serikali ya Afrika Kusini kuwaandaa polisi 41,000 kwaajili ya ulinzi wakati wa michuano hiyo.

source nifahamishe