Agundulika Bado Yu Hai, Akiwa Ndani ya Jeneza

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /


Babu mmoja mwenye umri wa miaka 76 wa nchini Poland amezinduka toka kuzimu sekunde chache kabla ya misumari kupigiliwa kwenye jeneza lake.
Babu Jozef Guzy mwenye umri wa miaka 76 ambaye ni mfugaji wa nyuki, alitangazwa amefariki kutokana na shambulio la moyo akiwa karibu na mizinga yake ya nyuki katika mji wa Katowise kusini mwa Poland.

Ambulansi iliitwa baada ya babu Jozef kukumbwa na shambulio la moyo na daktari mzoefu alitangaza baada ya kumpima kuwa Jozef ameishafariki.

"Jozef alikuwa hapumui, kulikuwa hakuna mapigo ya moyo na mwili wake ulikuwa wa baridi ambazo zote hizo ni dalili za kifo", Jerzy Wisniewski, msemaji wa ambulansi katika mji huo alisema.

Masaa matatu baada ya kutangazwa amefariki, watu wa mazishi walifika kuuchukua mwili wake.

Afisa wa mazishi, Dariusz Wysluchato aliuweka mwili wake kwenye jeneza na alikuwa kwenye hatua za mwisho za kulifunga jeneza wakati mkewe Jozef alipomtaka amvue saa aliyokuwa amevaa.

Wakati afisa huyo alipokuwa akimvua saa bila kutarajia alimgusa shingoni na kuhisi Jozef bado anapumua.

"Nilimgusa kwenye mshipa mkubwa wa damu kwenye shingo na ndipo nilipogundua kuwa hajafariki. Nilimpima tena kuhakikisha hajafariki na kuanza kupiga kelele kuita watu", alisema Dariusz.

Dariusz alimuita rafiki yake ambaye alihakikisha kuwa Jozef alikuwa akitoa pumzi hafifu sana.

Ambulansi iliitwa tena na daktari yule yule aliyesema amefariki, alimpima tena na kutangaza kuwa Jozef "amerudi toka kuzimu".

Jozef alipelekwa hospitali ambapo madaktari walishindwa kugundua ugonjwa unaomsumbua pamoja na kumfanyia vipimo kadhaa.

Baada ya kupumzishwa hospitalini kwa siku kadhaa, Jozef aliruhusiwa kurudi nyumbani kwake.

Jozef anasema kuwa kitu cha kwanza alichofanya baada ya kutoka hospitali ni kumpelekea Dariusz bakuli la asali kama shukurani kwa kuokoa maisha yake.

Tukio la Jozef limetokea ikiwa ni wiki moja tu baada ya mwanaume mmoja nchini China kutangazwa amefariki baada ya kupata ajali ya pili.

Mwanaume huyo aliyetajwa kama Zhang Houming, 46, Aliwekwa monchwari hospitalini lakini aligundulika kuwa bado yupo hai akitoa pumzi hafifu sana alipowekwa ndani ya jeneza.

Alirudishwa tena hospitali lakini alifariki lisaa limoja baadae.

Familia yake katika mji wa Neijiang imefungua kesi ya madai sawa na Tsh. Milioni 270 kama fidia.

source nifahamishe