Serikali kugharimia wanafunzi mitihani

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /

SERIKALI itatumia takribani Sh bilioni 20 mwaka ujao wa fedha kuendesha shughuli za mitihani baada ya kutangaza uamuzi wa kufuta ada ya mitihani ambayo ilikuwa ikigharimia shughuli hizo.

Uamuzi wa Serikali kubeba mzigo huo wa gharama, umetokana na kile kilichoelezwa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, kuwa ni kubaini kwamba maelfu ya wanafunzi walikuwa wakishindwa kufanya mitihani baada ya kukosa ada au fedha zao kutowasilishwa na wakuu wa shule.

Akizungumza na gazeti hili jana mjini hapa, Mahiza alisema kulingana na takwimu zilizopo za wanafunzi walioshindwa kufanya mitihani katika miaka ya nyuma, endapo uamuzi wa kufuta ada usingechukuliwa, zaidi ya wanafunzi 50,000 wa shule za Serikali wasingefanya mitihani.

“Miaka ya nyuma tumepoteza maelfu ya wanafunzi. Tusipofanya hivi zaidi ya wanafunzi 50,000 watapotea,” alisema.

Pamoja na Serikali kuamua kubeba jukumu hilo, Mahiza alisema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, ameagiza wanafunzi 29,000 wa kidato cha pili walioshindwa kufanya mtihani mwaka jana kwa kukosa ada, watafutwe na uandaliwe utaratibu utakaowawezesha kurudi shuleni. Amewaagiza wakaguzi kuanzia Februari mosi hadi 12 mwaka huu, wawaandalie utaratibu.

Mahiza ambaye alikuwa akizungumzia yaliyojiri katika mkutano wa watendaji wa kitaaluma ambako Waziri Maghembe alitamka uamuzi wa kufuta ada za mitihani, aliweka bayana takwimu za idadi ya wanafunzi walioshindwa kufanya mitihani tangu mwaka 2007 hadi mwaka jana.

Alisema mwaka 2007, wanafunzi 25,310 wa kidato cha pili hawakufanya mtihani; 3,870 kidato cha nne na 351 cha sita.

Mwaka juzi, ambao hawakufanya mtihani ni 17,970 cha pili, 3,500 cha nne na 251 cha sita.
Wanafunzi ambao hawakufanya mtihani mwaka jana ni 29,700 kidato cha pili, 3,500 cha nne. Kwa upande wa kidato cha sita, idadi haijajulikana kutokana na kwamba wanatarajiwa kufanya mtihani wiki ya pili ya mwezi ujao.

“Agizo hili haliwahusu wa kidato cha sita na hawawezi kurudishiwa ada walizotoa,” alisema Naibu Waziri.

Kwa mujibu wa Mahiza, Kanda ya Ziwa inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 8,000 wa kidato cha pili ambao hawakufanya mtihani wa kidato cha pili. Inafuatia Kanda ya Magharibi yenye wanafunzi 7,000.

Akielezea uamuzi wa kufuta ada hizo mwaka huu, Mahiza alisema dhamira ya kufanya hivyo ilianza mwaka 2007 walipobaini hali ilivyo.

Alisema lakini Serikali ilichelea kuchukua uamuzi kutokana na madeni mengi iliyokuwa ikidaiwa na walimu na wazabuni waliokuwa wakisambaza chakula katika shule na vyuo.

“Mwaka juzi tukaona bado kuna mzigo mkubwa. Ilipofika mwaka jana, tukaona kwamba kuna ahueni. Lakini tulichelewa kuingiza kwenye bajeti.“Mwaka huu sasa wizara haina mzigo mkubwa, madai yamelipwa na suala la chakula ni jukumu la Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),” alisema Mahiza.

Kuhusu mambo mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huo uliohusisha maofisa elimu, wakaguzi na wakuza mitaala, maofisa mitihani na watafiti, Mahiza alisema ni chimbuko la kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi.

“Utafiti umebaini kuna mambo mengi yanachangia, lakini kubwa ni uwajibikaji mdogo,” alisema. Alitoa mfano kwamba utafiti, ukiwamo wa Wizara uliofanywa tangu mwaka 2007 hadi mwaka juzi, ulibaini, kwamba walimu hawakamilishi mada zinazostahili kufundishwa, mahudhurio mabaya ya wanafunzi, uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ni mambo yanayochangia tatizo.

Kupitia mkutano huo, halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha zinafufua mfumo wa kutoa mafunzo kazini kupitia vituo vya mafunzo. Mitaala ya vyuo vya ualimu, hususan ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi pia itaboreshwa.

Naibu Waziri aliliambia gazeti hili kwamba yapo mambo mengi yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo kwa ajili ya kuboresha elimu nchini na kwamba umeandaliwa waraka utakaomwezesha Waziri Maghembe kutoa tamko rasmi juu ya yote yaliyojiri.

Katika hatua nyingine, Mahiza akijibu swali bungeni, alisema kamwe suala la madeni ya walimu halitakuwa tishio au fimbo dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa linashughulikiwa ipasavyo.

Mahiza alikuwa akijibu swali la nyongeza, la Mbunge wa Meatu, Salum Khamis Salum (CCM), aliyetaka kujua ni lini mchakato wa kuhakiki madai yote ya walimu utakamilika rasmi na kuitaka Serikali itoe jibu kamili kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinaweza kutumia ‘fimbo’ hiyo dhidi ya CCM.

Alisema walimu ni sehemu ya watumishi wa umma na wanaongozwa na taratibu na kanuni za utumishi wa umma, kutokana na hali hiyo, mchakato huo wa kuhakiki ni endelevu ili kila mtu apate haki yake.

“Kwa hili hakuna tishio la CWT kwa CCM hii ni haki yao kama watumishi kwa wale wanaostahili na CCM itashinda,” alisema Mahiza huku akishangiliwa na wabunge wa CCM.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), ambaye alitaka kufahamu ni walimu wangapi wamelipwa hadi sasa, Mahiza alisema baada ya kukamilika kwa mchakato wa uhakiki wa madeni ya walimu Februari mwaka jana, walimu 61,423 walilipwa huku 14,215 madai yao yakikataliwa.

Alisema walimu ambao madai yao yalikataliwa ni kutokana na kutofuata taratibu, kughushi nyaraka na kukosa vielelezo.

source habari leo