Mtoto Aliyezaliwa Akiwa na Miguu Minne, Mikono Minne Aanza Shule

Friday, January 29, 2010 / Posted by ishak /Mtoto wa nchini India ambaye alizaliwa akiwa na miguu minne na mikono minne, ameanza shule miaka miwili baada ya kufanyiwa operesheni ya kuviondoa viungo vilivyozidi.
Lakshmi Tatma alichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari alipozaliwa katika mji wa Bihar nchini India miaka minne iliyopita akiwa na miguu minne na mikono minne.

Lakshmi alizaliwa mwili wake ukiwa umeungana kuanzia kiunoni na pacha mwenzake ambaye alikuwa hana kichwa na hivyo kumfanya awe na jumla ya miguu minne na mikono minne.

Wakati huo kutokana na maumbile yake ya ajabu Lakshmi alikuwa akiabudiwa kama mungu wa kihindu.

Baada ya operesheni kubwa iliyofanyika miaka miwili iliyopita ambayo ilimalizika kwa mafanikio makubwa, miguu na mikono iliyozidi kwenye kiwiliwili chake iliondolewa.

Hivi sasa Lakshmi ametimiza miaka minne na ameanza shule sambamba na watoto wenzake.

"Nikifikiria jinsi alivyokuwa, sikutegemea Lakshmi angeweza kwenda shule au angekuwa na maisha aliyo nayo sasa", alisema mama yake Poonam, mwenye umri wa miaka 26.

"Vitu vyote ambavyo anaweza kuvifanya sasa alikuwa hawezi kuvifanya kabla ya operesheni, alikuwa hawezi hata kukaa lakini sasa anaweza hata kukimbia na kucheza na watoto wenzake", aliendelea kusema mama yake.

Lakshmi pamoja na kwamba hivi sasa amepona kabisa bado anahitajika kufanyiwa operesheni zaidi baada jinsi anavyozidi kukua ili kuvirekebisha viungo vyake.


source nifahamishe