Ronaldo Amvunja Pua Mchezaji Mwenzake

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /


Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo aliifungia timu yake magoli mawili ya ushindi dhidi ya timu ya Malaga lakini alitolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu baada ya kumvunja pua mchezaji wa Malaga.
Cristiano Ronaldo alibaki akitoa lawama zake kwa refa aliyemtupa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu alipoivunja pua ya beki wa Malaga, Patrick Mtiliga.

Ronaldo ambaye ndiye mchezaji ghali kuliko wote duniani, aliifungia Real Madrid magoli yote mawili yaliyoipa ushindi wa mabao 2-0 katika mechi hiyo ya jumapili jioni na kulifanya pengo la pointi kati yake na Barcelona kufikia pointi tano.

Ronaldo alikuwa akikokota mpira kwenye dakika ya 70 akijaribu kumtoka Mtiliga na ndipo alipouzungusha mkono wake mara mbili na kumgonga puani Mtiliga na kupelekea kuvunjika kwa pua yake.

Kocha wa Malaga, Juan Ramon Lopez Muniz alilaani kitendo cha Ronaldo na alisema kuwa Mtiliga atatumia wiki tatu nje ya uwanja akiuguza pua yake.

Ronaldo alitoka nje ya uwanja huku akitoa lawama zake kwa refa wa mechi hiyo akisema kuwa hakustahili kadi nyekundu.

"Watu wanaojua mpira wanajua nia yangu kuwa ilikuwa ni kuwania mpira", alilama Ronadlo.

"Najua mmeona damu mmlipoangalia kwenye TV lakini ukweli ni kwamba nilikuwa nacheza mpira tu sikuwa na nia ya kumuumiza mtu yoyote", aliendelea kusema Ronaldo.

Ronaldo aliendelea kusema kuwa alimfuata Mtiliga baada ya mechi na kumuomba radhi.

source nifahamishe