Msoma mita wa Dawasco afikishwa mahamani kwa kuomba rushwa

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /

MSOMA mita wa Kampuni ya kusambaza maji safi jijini Dar es Salaam (Dawasco), Chobines Mabega (38), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinonondoni, kwa tuhuma za kuomba hongo.
Mabega alisomewa mashitaka mawili na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB), Ronald Manyiri mbele ya hakimu Sundi Fimbo wa mahakama hiyo.

Manyiri alidai kuwa mtuhumiwa anakabiliwa na mashtaka mawili yote yakiwa ni ya kuomba hongo kinyume na sheria za nchi.

Akisoma hati hiyo alidai kuwa Januari 20 , mwaka huu huko eneo la Mikocheni katika Hotel ya Keys, mtuhumiwa ambaye ni mwajiriwa wa Dawasco aliomba rushwa ya shilingi milioni 1,500,000 kwa mlalamikaji kama kishawishi cha kutomchukulia hatua za kisheria kwa kuunganisha maji kinyume cha utaratibu.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Januari 22, katika maeneo ya Bar Blue Star, mtuhumiwa alimshawishi mtu mwingine ampatie kiasi cha shilingi 750,000 zikiwa ni sehemu ya hongo kutoka Kinabo Masawe kwa kuwa aliunganisha maji kinyume na sheria na alimtishia ampatie kiasi hicho ili aweze kumrekebishia pasipo na mamlaka kujua.

Mtuhumiwa huyo alipotakiwa kujibu mashitaka hayo alikana hakuhusika na yupo nje kwa dhamana na kesi hiyo iliahirishwa hadi Februali 16 mwaka huu.


source.nifahamishe