Kuelekea uchaguzi mkuu: Idadi ya wabunge kuongezwa

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /


HATIMAYE Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetangaza mpango ambao utaweza kuondoa misuguano ndani ya vyama kwenye baadhi ya majimbo baada ya kueleza uwezekano wa kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.

Tayari misuguano imeshaanza kuonekana kwenye baadhi ya vyama, na hasa tawala kutokana na wanachama wake kutangaza nia yao ya kuwania ubunge kwenye majimbo ambayo kwa sasa yanashikiliwa na wabunge kutoka chama chao, hali inayoashiria uwezekano wa kuwepo na vita kali ya ubunge.

Lakini Nec jana ilitangaza kuwa itafanya uchunguzi kuona kama kuna haja ya kuongeza majimbo kabla ya uchaguzi mkuu ujao kama sheria inavyoipa tume hiyo mamlaka ya kugawa majimbo kila baada ya miaka kumi.

Bunge la sasa la Jamhuri ya Muungano lina wabunge 323 ambao wakiingia kwenye ukumbi wao mjini Dodoma ambao una uwezo wa kuchukua watu 346, kunakuwa na upungufu wa watu 23.

Mbali na kutangaza nia hiyo ya kuongeza idadi ya majimbo, Nec jana iliweka wazi kwamba mchakato mzima wa uchaguzi huo, utagharimu Sh64 bilioni.

Makamu mwenyekiti wa Nec, Jaji Omar Makungu alisema jana kuwa majimbo hayo yataongezwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1977 ambayo imeipa tume hiyo mamlaka ya kuchunguza mipaka na kugawa majimbo kila baada ya miaka kumi.

"Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ya 1977, Nec imepewa mamlaka ya kuchunguza mipaka na kuigawa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge," alisema alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

"Aidha kwa mujibu wa katiba hiyo, tume inatakiwa kufanya uchunguzi wa mipaka na kugawa majimbo mara kwa mara au angalau kila baada ya miaka kumi."

Alisema: "Kwa kuzingatia matakwa hayo, Nec inatarajia kufanya uchunguzi wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi na kugawa majimbo kama itahitajika kabla ya uchaguzi mkuu ujao."

Jaji alitaja vigezo 12 vitakavyotumika kugawa majimbo hayo kuwa ni pamoja na mawasiliano, hali ya kijiografia, idadi ya watu, idadi ya watu ambayo inatokana na makasio ya ongezeko la watu hadi mwaka 2008 na inayotokana na sensa ya mwaka 2002.

"Mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu ndiyo kigezo kikuu na cha kwanza katika kuamua majimbo gani yagawanywe. Takwimu za idadi ya watu zitakazotumika zimepatikana kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu," alisema Jaji Makungu.

"Pia idadi ya watu katika jimbo inapatikana kwa kuchukua idadi ya watu wote nchi nzima kugawanya kwa idadi ya majimbo yaliyopo ambayo ni 232. Ambapo idadi ya watu katika majimbo ya uchaguzi vijijini ni 206,130 na mijini ni 237,937."

Vigezo vingine ni hali ya kiuchumi ambacho hutumia ukusanyaji wa mapato katika eneo husika.

"Hapa uangalifu utachukuliwa ili maeneo ambayo yako juu sana kiuchumi yasimeze kiuwakilishi maeneo yaliyo chini kiuchumi. maeneo yaliyochini kiuchumi yatafikiriwa," alisema.

Vigezo vingine ni ukubwa wa eneo la jimbo, mipaka ya kiutawala, jimbo moja lisiwe ndani ya wilaya ua halmashauri mbili, kata moja isiwe ndani ya majimbo mawili ya uchaguzi.

Vingine ni mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya Muungano baina ya Bara na Visiwani, uwezo wa ukumbi wa Bunge pamoja na viti maalum vya wanawake.

"Katiba imetenga kiasi kisichopungua asilimia 30 kwa ajili ya wabunge wanawake wa viti maalum ili kuweka usawa wa kijinsia japokuwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka," alisema.

Jaji Makungu alisema maombi, maoni na mapendekezo ya kugawa kwa majimbo au kuchuguza yanatakiwa yawasilishwe kwa mkurugenzi wa halmashauri husika na yatajadiliwa katika vikao rasmi.

"Mwisho wa NEC kupokea maombi ni Februari 28 mwaka huu na tutafanya uchambuzi kisha mashauriano na halmashauri husika kabla ya kufikia uamuzi. Tume inatarajia kukamilisha zoezi hili mwezi Aprili," alisema.

Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashillilah aliliambia gazeti hili baadaye jana kuwa Bunge lina uwezo wa kuchukua wabunge 346 tu kwa wakati mmoja. Kwa sasa Bunge lina wabunge 323.

"Ukumbi wa Bunge letu una uwezo wa kubeba watu 346 tu sasa kuna wabunge 323," alisema Dk Kashillilah alipoulizwa na gazeti hili kufafanua suala hilo.

Akizungumzia katika mkutano huo wa waandishi wa habari mkurugenzi wa Uchaguzi Rajab Kiravu alisema kazi ya kuchunguza mipaka na ugawaji wa majimbo hayo itagharimu Sh50 milioni.

Kiravu alisema gharama zote za mchakato wa uchaguzi huo zitakuwa Sh64 bilioni ikiwa ni nyongeza ya Sh3 bilioni ikilinganishwa na gharama zilizotumika katika uchaguzi wa mwaka 2005.


source mwananchi