Binamu wa Saddam Hussein Anyongwa

Tuesday, January 26, 2010 / Posted by ishak /


Binamu wa rais wa zamani wa Iraq na mpambe wa karibu wa Saddam Hussein, Ali Hassan al-Majid au maarufu kama "Chemical Ali" amenyongwa leo kwa makosa ya mauji aliyofanya wakati wa utawala wa rais Saddam.
Ali Hassan al-Majid au maarufu kama "Chemical Ali" amenyongwa leo kufuatia hukumu ya kunyongwa iliyotolewa wiki iliyopita na mahakama kuu ya nchini Iraq.

"Chemical Ali" anatuhumiwa kuwaua kwa kutumia gesi za sumu zaidi ya wakurdi 5,000 mnamo mwaka 1988.

Ali alinyongwa kwa kitanzi katika staili ile ile ambayo Saddam Hussein alinyongwa miaka mitano iliyopita.

"Adhabu ya kifo ya Ali Hassan al-Majid imeishatekelezwa", alisema Ali al-Dabbagh, msemaji wa serikali ya Iraq.

Ali aliyekuwa na umri wa miaka 68 alihukumiwa kunyongwa januari 17 mwaka huu kwa makosa ya kuamuru gesi ya sumu itumike kuwaua wakurdi zaidi ya 5,000 katika mji wa Halabja karibu na mpaka wa Iran. Maafisa wengine wa serikali ya Iraq walihukumiwa vifungo vya miaka mingi jela kwa kushiriki katika mauaji hayo.

Kabla ya kuhukumiwa kunyongwa wiki iliyopita, Ali alikuwa ameishahukumiwa kunyongwa mara tatu kwa mauaji ya wakurdi kwenye miaka ya 1980 na mauaji ya waislamu wa dhehebu la Shia kwenye miaka ya 1990.

Ali alibatizwa jina la "Chemical Ali" na wakurdi ambao pia walikuwa wakimuita "Butcher of Kurdistan".

Ali alikamatwa mwaka 2003 baada ya kuangushwa kwa serikali ya Iraq na Marekani.


source nifahamishe