Akasirishwa na Gredi ya Masomo Yake, Amuua Mwalimu Wake

Monday, February 22, 2010 / Posted by ishak /


Mwanafunzi mmoja nchini Ujerumani aliyekasirishwa na gredi ya masomo yake, ameivamia shule yake na kuwashambulia walimu wake na kumuua mwalimu wake mmoja kwa kumcharanga na kisu.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea kwenye shule yenye wanafunzi 3200 ya Technik II katika maeneo ya Mundenheim ya mji wa Ludwigshafen nchini Ujerumani.

Mtuhumiwa aliyejulikana kwa jina la Florian K mwenye umri wa miaka 23 alirudi tena kwenye shule hiyo ambayo alihitimu masomo yake mwaka 2004 akiwa na kisu kikubwa na bastola kwa nia ya kufanya mauaji makubwa ya walimu wake.

Mwalimu Rudolf B. mwenye umri wa miaka 58 ambaye alimfundisha somo la hisabati Florian alifariki kwenye eneo la tukio baada ya kuchomwachomwa na kisu na Florian ambaye alikamatwa muda mfupi baada ya kufanya mauaji hayo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Florian alikuwa amepanga kufanya mauaji makubwa sana kwenye shule, alikutana na mwalimu Rudolf kwenye ngazi na ndipo alipotimiza azma yake hiyo.

Florian ambaye alikuwa akipiga risasi hovyo aliwajeruhi walimu watatu kabla ya kuwekwa chini ya ulinzi na timu maalumu ya polisi iliyoitwa kwenye shule hiyo yenye walimu 130.

Florian alikiri kuwa alikuwa amepanga kuwaua walimu wote waliosababisha amalize shule akiwa na gredi ya chini.

Taarifa zaidi zilizotolewa zilisema kuwa Florian aliacha ujumbe kwenye internet kuhusiana na mipango yake ya kuwaua walimu wake aliweka video za mazoezi yake ya kutumia bunduki kwenye tovuti moja ya video ya Ujerumani.

Pia Florian aliandika katika tovuti moja kuwa mwaka wake wa kufariki ni mwaka 2010 na siku yake ya kufariki ni ndiyo siku hiyo ambayo alifanya mashambulizi hayo.

source nifahamishe