Apigania Atambulike Kuwa Yeye Ndiye Mtu Mfupi Duniani

Monday, February 22, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mwenye urefu wa sentimeta 56 tu toka nchini Nepal ameondoka nchini kwake na kuanza safari za kuzunguka nchi kadhaa akitaka atambulike kuwa yeye ndiye mtu mfupi kuliko wote duniani.
Khagendra Thapa Magar ameanza safari za kutembelea nchi za ulaya kupiga kampeni za kuingizwa kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness kuwa yeye ndiye mtu mfupi kuliko wote duniani.

Khagendra alituma maombi yake kwenye ofisi za London nchini Uingereza akitaka aingizwe kwenye rekodi za dunia pindi afikapo umri wa miaka 18 mwezi oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, Khagendra amesema kuwa hajapata majibu yoyote toka kwenye ofisi hiyo.

Awali Khagendra alituma maombi yake ya kuingizwa kwenye rekodi za dunia alipokuwa na umri wa miaka 14 lakini maombi yake yalitupiliwa mbali kwasababu hajatimiza umri wa miaka 18 wa kumwezesha ahesabike kama mtu mzima huku ikihofiwa kuwa anaweza kurefuka.

Madaktari nchini Nepal wameshindwa kuelezea sababu zinazomfanya Khagendra awe mfupi kiasi hicho.

"Tunaenda Italia kujaribu kuingiza jina lake kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness " alisema baba yake Rup Bahadur Thapa Magar, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kabla ya kuanza safari toka mjini Katmandu.

Baada ya kutoka nchini Italia ambako watashiriki kwenye shoo moja kwenye Televisheni ya Italia, Khagendra na kambi yake wataamua nchi gani nyingine ya kwenda.

Mamia ya wapenzi wa Khagendra walijitokeza jana kumuaga na kumkabidhi mashada ya maua.

Hivi sasa He Pingping wa nchini China, ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia ya mtu mfupi kuliko wote duniani akiwa na urefu wa sentimeta 73.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment