Mjerumani Aponzwa na Mbwa Wake

Wednesday, February 24, 2010 / Posted by ishak /


Mjerumani aliyekuwa akiwakimbia polisi na kujificha kwenye kabati ndani ya nyumba yake, aliponzwa na mbwa wake aliyewaongoza polisi hadi kwenye sehemu aliyojificha.
Mwanaume mmoja wa nchini Ujerumani aliponzwa na mbwa wake mwenyewe baada ya kuwakimbia polisi waliofika nyumbani kwake na kwenda kujificha kwenye kabati la nguo.

Wakati polisi walipogonga mlango wa nyumba yake iliyopo kwenye kitongoji cha Euskirchen karibu na mji wa Cologne, mlango ulifunguliwa na mwanaume mwingine ambaye alisema hajui mwanaume anayetafutwa ameenda wapi.

Lakini mwanaume huyo alipomuachia mbwa aliyekuwa amemshikilia, mbwa huyo moja kwa moja alienda kwenye kabati alilojificha mmiliki wake na kuanza kutingisha mkia.

Kitendo hicho kiliwashtua polisi ambao waliamua kulisachi kabati hilo lenye unene wa mita moja na urefu wa sentimeta 80.

Polisi walipolifungua kabati hilo, Mwanaume huyo alikutwa amejikunja ndani yake. Walimkamata na kumtia mbaroni.

Polisi hawakusema walikuwa wakimtafuta mwanaume huyo kwa kosa gani na walikataa kutaja umri wala jina la mtuhumiwa huyo.

source nifahamishe