Babu wa Miaka 97 Ashinda Bahati Nasibu

Wednesday, February 24, 2010 / Posted by ishak /


Babu aliyepigika na umaskini maisha yake yote ameuaga umaskini akiwa na umri wa miaka 97 baada ya kushinda bahati nasibu ya mamilioni ya pesa.
Babu mmoja wa nchini Vitenam aliyeteseka na maisha ya umaskini miaka nenda miaka rudi, amegeuka tajiri ghafla baada ya kushinda bahati nasibu na kujipatia dola 400,000 (Zaidi ya Tsh. Milioni 500).

Taarifa zimesema kuwa muda mfupi baada ya babu huyo kushinda bahati nasibu mzozo mkubwa umezuka baina ya ndugu zake wanaowania angalau urithi wa mali zake.

Jirani mmoja wa babu huyo wa mji wa Ho Chi Minh kusini mwa Vietnam alisema kuwa ilimbidi aingilie kati kumzuia babu huyo asiendelee kuzigawa pesa zake kwa mamia ya watu waliojazana kwenye nyumba yake.

Pesa zake zote zilizobakia zilipelekwa kuhifadhiwa benki, liliripoti gazeti la Thanh Nien la Vietnam.

Mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Nguyen Van Het alishinda bahati nasibu hiyo baada ya kununua tiketi ya bahati nasibu kwa kutumia pesa alizopewa siku ya mwaka mpya kama zawadi.

Het amejishindia kiasi cha dong za Vietnam bilioni 7.6 ambazo ni sawa na dola za kimarekani laki nne.

Afisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa ilibidi wazizuie pesa za Het na kumwekea benki baada ya mamia ya ndugu na jamaa kujazana kwenye nyumba yake wakiomba pesa.

"Tutasubiria wiki kadhaa ili aweze kutulia ndipo tutakapomuuliza anataka kuzifanyia nini pesa zake", alisema afisa huyo.

source nifahamishe