Akataliwa Kubadili Dini, Atishia Kujiua

Sunday, January 31, 2010 / Posted by ishak /

MSICHANA mmoja [24] [jina kapuni] mkazi wa Mikocheni B, mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amejikuta akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuitaarifu familia yake kuwa atakunywa sumu baada ya kukataliwa na wazazi wake kubadili dini ili aoane na mpenzi wake.
Chanzo chetu cha habari kilisema kuwa kasheshe lilianza baada ya msichana huyo kuwataarifu wazazi wake kuwa amepata mchumba na yuko tayari kubadili dini yake ili aweze kuoana naye.

Lakini wazazi wake walimkatalia kwa kuwa walikuwa wametofautiana kwa imani za kidini.

Wazazi wa msichana huyo waliweka wazi kuwa hawako tayari kuona binti yao akibadili dini ili aone na mpenzi wake huyo.

Msichana huyo alionekana kutoridhika na uamuzi wa wazazi wake hao na baada ya siku chache kupita aliwaambia wazazi wake hao kuwa hataweza kumkosa mpenzi wake huyo aliyempenda kwa moyo wake wote na kwa kuwa hawataki aoane naye basi atakunywa sumu ili aiage dunia.

Kutokana na tamko hilo kikao cha dharura cha familia kiliitishwa na walio wengi katika kikao hicho walitoa tamko kuwa hawako tayari ndugu yao abadili dini.

Msichana huyo naye alitoa tamko mbele ya kikao hicho kuwa atakunywa sumu pamoja na baadhi ya wanafamilia kumsihi asifanye hivyo kwa kuwa angeweza kupata mchumba mwingine wa dni yake.

Msichana huyo aliingia chumbani kwake akitishia kutafuta sumu ili ajiue na kupelekea baadhi ya wanafamilia kwenda kutoa tarifa kituo cha polisi.

Polisi walimkamata msichana huyo na kumpeleka kituoni huku wazazi wake na wanafamilia wengine wakiitisha kikao kingine kujadili sakata hilo.

source nifahamishe