Mafundi wafa kwa kufunikwa na kifusi Dar

Friday, February 05, 2010 / Posted by ishak /

MAFUNDI UJENZI wawili wakazi wa Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, wamekufa papo hapo baada ya kufunikwa na kifusi cha mchanga walichokichimba kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi
Taarifa hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, na kusema tukio hilo lilitokea juzi huko Pugu Bagdad.

Shilogile amesema kuwa, mafundi hao James Katenga (27) na Adamu Mtolela (30), walikutwa na umauti huo wakati wakiendelea na uchimbaji mchanga kwenye moja ya machimbo yaliyopo eneo hilo.

Amesema mafundi hao walikutwa na wenzi wao ambao walikuwa wanahusika katika ujenzi na kuwakuta wameshapoteza maisha na kutoa tarifa kituo cha polisi.

Katika tukio jingine la ajali lililotokea jijini Dar es Salaam, mtu mmoja amekufa dunia papohapo na mwenzake kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari.

Amesema mtu aliyefariki alitambulika kwa jina la Mussa Issah (24) ambaye alikuwa akiendesha pikipiki na aliyejeruhiwa alikuwa ni abiria wake aliyetambuliwa kwa jina la Gidimash Geofrey 22 .

Amesema waligongwa vibaya na gari dogo aina ya Audi Saloon eneo la Brush huko barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Liberatus Sabas, alisema ajali hiyo ilitokea juzi eneo hilo wakati gari hilo lenye namba za usajili T 357 ASE likiendeshwa na Magreth Lega (34).

Amesema gari hilo lilikuwa alikitokea eneo la Kamata kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati dereva wa pikipiki hiyo yenye namba za usajili T 391 AYU alikuwa akitokea Tazara kuelekea Kamata.

Amesema Geofrey amelazwa hospitali ya Temeke.

source nifahamishe