Jerry Muro na sakata lake la rushwa..............

Sunday, January 31, 2010 / Posted by ishak /




Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Mtangazaji wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) Jerry Muro (pichani juu kulia) kwa tuhuma za kudai fedha kwa njia ya vitisho.

Muro anadaiwa kumtisha aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo Michael Wage ambaye hivi karibuni alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa tuhuma za ubadhilifu pamoja na viongozi wengine wa Halmahauri ya Wilaya Bagamoyo.

Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Suleimani Kova alikiri jeshi lake kumshikilia Muro na kuwa alimtishia Wage kuwa yeye ni Ofisa wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na kumtaka atoe fedha Sh milioni 10.

“Polisi inamhoji Muro dhidi ya tuhuma hizo na mahojiano yakikamilika taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na maelezo zaidi nitayatoa kesho wakati wa mazungumzo yangu na waandishi wa habari” Kova alisema.

Aidha blogu ya Watu ilimwona Bingwa huyo wa Tuzo za Uandishi wa Habari 2009 Tanzania akiwa polisi na mkononi ameshikilia bahasha tatu pamoja na kamera ya Video.

Ilipomhoji juu ya kuhusika na tuhuma hizo alikana na kudai kushangazwa kuwekwa chini ya ulinzi kwa madai kuwa alipigiwa simu na mtu kupewa taarifa kuwa kuna kazi katika Hoteli ya City Garden.

“Kaka nilitaarifiwa tu kama ujuavyo kazi zetu kuwa kuna kazi City Garden niakaamua kwenda, lakini baada ya kufika tu nilishangaa nawekwa chini ya ulinzi na askari kanzu ambao ndiyo walionifikisha kituoni hapa bila ya kunitajia kosa lanmgu. ” alilonga Muro.

Kwa upande wake Wage alidai kuwa mtuhumiwa anatumiwa na watu wengine ambapo juzi alimpandisha katika gari lake na kumfunga pingu kisha kumtaka atoe Sh milioni 10 na kwa kuthibitisha kuwa alikuwa ndani ya gari hilo alidai kuacha miwani yake yenye mikanda myeusi.

Polisi ilipomhoji Muro kama anazo pingu alikiri kumiliki pingu pamoja na bastola ambapo baada upekuzi katika gari lake lenye namba za usajili T 545 BEH polisi walikuta pingu hizo pamoja miwani iliyosemwa na mlalamikaji.

Muro ameibuka kuwa mtangazaji mahari kwa mwaka 2009 hadi kujinyakulia tuzo ya Mwandishi bora wa mwaka kupitia vipindi vyake vya Televisheni vya USIKU WA HABARI vinavyorushwa katika kituo cha TBC1 kila siku na kabla ya kuhamia hapo alikuwa kituo cha ITV na aliendesha kipindi cha RIPOTI MAALUM.

Miongoni mwa mambo aliyokuwa akirusha katika vipindi hivyo ni pamoja na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na ukiukwaji wa sheria.

Polisi ni wahanga wakuu katika vipindi hivyo kwani mara mbili amewatoa Polisi Usalama barabarani wakiomba na kupokea rushwa hadharani kutoka kwa madereva wa malori na mabasi ya mikoani.

0 comments:

Post a Comment