Msichana Azikwa Hai Kwa Kosa la Kuwa na Rafiki wa Kiume

Friday, February 05, 2010 / Posted by ishak /


Msichana mwenye umri wa miaka 16 amezikwa hai na ndugu zake nchini Uturuki kwa kosa la kuwa na rafiki wa kiume hivyo kudaiwa ameiletea aibu familia yake.
Msichana mwenye umri wa miaka 16 wa nchini Uturuki amezikwa hai na ndugu zake baada ya kushutumiwa kuwa ameitia aibu familia yake kwa kuwa na marafiki wa kiume.

Baada ya kupewa taarifa ya tukio hilo, polisi walifanikiwa kuupata mwili wa msichana huyo aliyetambulika kwa jina la Medine Memi siku 40 baada ya kutangazwa kuwa ametoweka.

Mwili wa Medine ulikutwa katika mji wa Adiyaman umekalishwa kitako kwenye shimo la mita 2 huku mikono yake ikiwa imefungwa na kamba.

Baada ya maiti yake kufanyiwa vipimo kadhaa iligundulika kuwa kwenye tumbo lake na mapafu kulikuwa na kiasi cha mchanga hivyo kumaanisha kuwa alizikwa akiwa hai, taarifa ya wataalamu wa makosa ya jinai ilisema.

"Matokeo ya uchunguzi wa maiti yake yanasikitisha sana, msichana ambaye hakuwa na mchubuko hata mmoja kwenye mwili wake na wala hakuwa na kiasi chochote cha sumu kwenye damu yake, alikuwa hai na mwenye kujitambua wakati alipozikwa hai", alisema mtaalamu mmoja ambaye hakutaka kusema jina lake.

Baba yake Medine na babu yake, wametiwa mbaroni na kutupwa jela wakati uchunguzi wa mauaji yake ukiendelea.

Shirika la habari la Anatolia la Uturuki liliripoti kuwa baba yake Meline alisema katika ushahidi wake polisi kuwa familia yake haikuwa ikifurahia kumuona Medine akiwa na marafiki wa kiume.

Mauaji hayo yanayoitwa "Mauaji ya kulinda heshima" hufanyika sana kusini mashariki mwa Uturuki katika maeneo yenye Wakurdi wengi.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikijaribu kuyakomesha mauaji hayo ya kulinda heshima bila mfanikio yoyote.

Wanawake wanaobakwa au wanaopata ujauzito kabla ya kuolewa huuliwa na familia zao katika kile kinachodaiwa kusafisha nuksi na fedheha wanazoziletea familia zao.

source nifahamishe

1 comments:

Comment by Ney on February 7, 2010 at 9:11 AM

ukatili mkubwa.

Post a Comment