Ana Miaka 13 Lakini Anaonekana Kama Bibi wa Miaka 50

Wednesday, February 03, 2010 / Posted by ishak /


Akikuambia kuwa ana umri wa miaka 13 unaweza ukabisha mpaka siku inayofuatia bila kukubali, msichana Zara Hartshorn wa nchini Uingereza aliyepatwa na ugonjwa wa ajabu anashindwa kuufaidi utoto wake kutokana na jinsi watu wanavyomchukulia kuwa yeye ni bibi mwenye umri wa miaka zaidi ya 50
Siku moja Zara Hartshorn alipanda basi la abiria na kutaka kukata tiketi ya watoto lakini dereva wa basi hilo alimuangalia kwa mshangao na kumwambia kuwa asifanye masihara alipe pesa kamili.

Zara aliposema kuwa yeye ni mtoto na ana umri wa miaka 13, dereva huyo ambaye alikuwa ni mzee wa makamo, alicheka sana na kumwambia kama ndio hivyo basi na mimi nina umri wa miaka 21.

Abiria nao waliingia kwenye mjadala huo na kumuunga mkono dereva kuwa Zara anawachezea watu akili kwani anaonekana wazi kuwa yeye ni kikongwe mwenye wajukuu.

Zara kwa aibu alishuka toka kwenye basi hilo na kusubiria basi jingine kwa imani dereva wa basi lifuatalo angeweza kumuelewa kuwa yeye ni mtoto.

Huo ni mkasa mdogo sana kati ya mikasa inayomkumba binti Zara Hartshorn wa Rotherham nchini Uingereza ambaye umri wake halisi ni miaka 13 pamoja na kwamba anaonekana kuwa na umri zaidi ya miaka 50.

Zara anakabiliwa na ugonjwa unaoitwa lipodystrophy ambao humfanya aonekane mzee sana kuliko umri wake huku akiwa na tabia za kitoto kama watoto wenzake.

Mama yake Zara bi Tracey Pollard ilibidi achukue uamuzi wa kumsimamisha masomo Zara kwakuwa alikuwa akitaniwa sana na wenzake akiitwa "Bibi" na kubandikwa majina kadhaa ya fedheha.

Ugonjwa unaomkabili Zara umewahi kuwatokea watu 2,000 tu duniani ambapo tabaka la chini la mafuta la ngozi hutoweka na kuifanya ngozi izeeke kwa spidi ya ajabu sana.

Ugonjwa wa lipodystrophy hauna tiba hivyo Zara ataendelea kuzeeka mapema jinsi anavyozidi kuendelea kukua.

Zara amerithi ugonjwa huo toka kwa mama yake ambaye ni miongoni mwa wagonjwa wachache sana duniani wa ugonjwa huo.

"Nilijuta kumzaa Zara, nilihuzunishwa sana nikifikiria kuwa Zara atapitia matatizo yote yaliyonikumba mimi wakati wa utoto wangu", alisema mama yake Zara.

Zara anaelezea masikitiko yake kutokana na jinsi watu wanavyomchukulia na kumtania kwa kusema kuwa wakati mwingine hukimbilia chumbani kwake na kuanza kulia peke yake.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment