Sigara Yamlipukia Mdomoni na Kumng'oa Meno Sita

Wednesday, February 03, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja wa nchini Indonesia ameapa kutokurudia tena kuvuta sigara baada ya sigara aliyokuwa akivuta kumlipukia mdomoni katika mazingira yasiyoeleweka na kusababisha meno yake sita yang'oke.
Andi Susanto mwenye umri wa miaka 31, anapatiwa matibabu hivi sasa kufuatia tukio la kupoteza meno yake sita ya mbele baada ya sigara kumlipukia mdomoni.

Akihojiwa na televisheni ya Metro TV ya Indonesia akiwa kwenye kitanda chake hospitalini, Andi alisema kuwa haelewi ilikuwaje sigara ikamlipukia mdomoni.

Andi alisema kuwa kampuni iliyozalisha sigara hiyo, inayoitwa PT Nojorono Tobacco Indonesia imekubali kulipa gharama zote za matibabu yake.

"Maafisa wa kampuni wameongea na familia yangu na wamekubali tumalize suala hili nje ya mahakama", alisema Andi.

Sababu ya mlipuko wa sigara hiyo bado haujajulikana na Andi anasema kuwa hakuwa akitafuna wala kuweka mdomoni kitu kingine chochote zaidi ya hiyo sigara.

Andi aliendelea kusema kuwa wakati alipoiwasha na kuanza kuivuta sigara hiyo inayoitwa "Clas Mild" hakuona utofauti wowote katika ladha au harufu lakini ghafla ililipuka na kuuharibu mdomo wake na kusababisha meno yake sita yang'oke.

Andi aliapa kuwa hataendelea kuvuta sigara tena atakaporuhusiwa kurudi nyumbani kwake toka hospitali.

Indonesia ni miongoni mwa nchi zenye biashara kubwa ya sigara na asilimia 60 ya wanaume wa Indonesia wanavuta sigara.

source nifahamishe