Serikali ya mseto yapitishwa Z'bar

Sunday, January 31, 2010 / Posted by ishak /

HATIMAE Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeidhiria hoja ya kuundwa kwa serikali ya kitaifa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Hoja hiyo liyowasilishwa na kiongozi wa kambi ya upinzani Abubakar Khamis Bakari na inayotaka kuundwa kwa serikali hiyo ili kujenga umoja na maridhiano kwa Wazanzibari ambayo wamekuwa katika migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu.

Wajumbe wa baraza hilo wote kwa sauti moja walikubaliana na suala hilo kwa kuridhia baaada ya Baraza la Wawakilishi kuwasilisha mapendekezo ya hoja binafsi ya Chama cha wananchi CUF na kujadiliwa na Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mgogoni Pemba.

Hata hivyo kabla ya kufanyika kwa mabadiliko hayo CUF walikubali kufanya mabadiliko katika hoja zake kadhaa baada ya wajumbe wa CCM kutaka kufanyiwa mabadiko hayo ya hoja yake.

"Marekebisho ya sheria ya uchaguzi, hatua ya kutaka ridhaa ya wananchi kwa njia ya kura ya maoni, na maekebisho ya katiba endapo wananchi wataridhia uanzishwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, yote hayo yafanywe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010," ilisema kipengele hicho ambacho kimekubaliwa na wote.

Katibu wa baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee akisoma vipengele vilivyoridhiwa na baraza hilo alisema ni pamoja na kukubaliwa kuundwa kwa kamati ya wajumbe sita ambao watasimamia suala hilo watatu wataotoka upinzani na serikalini.

Aidha Baraza hilo alisema limekubali suala la wakuu wa mikoa waendelee kuwa wanasiasa, lakini bado wateuliwe na rais kwa kufuata uwiano wa kura za rais za vyama viliomo kwenye Baraza kwa vyama vya siasa vilivyomo humo ama waondolewe kabisa katika vyama vya siasa ili wasiwe wateuliwa wa Rais.

Nafasi ya makamu wa rais ambayo ilikuwa na utata kidogo baada baadhi ya wajumbe kuwa na wasi wasi nayo juu ya mfumo utakaotumika kuunda nafasi hiyo bila ya kuingilia vipengele vya katiba vya muungano.

Hoja hizo zilizuka baada ya wajumbe hao kuuliza iwapo nafasi hiyo ikaleta utata wa kisheria katika katiba ya muungano kwa kuwa tayari nafasi hiyo imetajwa katika nafasi ya muungano na haitawezekana kuwa makamu wa pili kutoka Zanzibar.

Hoja nyingine kuhusu suala hilo kuwepo utata pindi rais aliteteuliwa pamoja na wateuliwa wengine wakiwewa pingamizi kwa mujibu wa tume ya uchaguzi je nafasi hiyo itaweza kupatikana hivi ambapo upande wa upinzani wanapendekeza suala hilo lipelekwe kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi kwa ajili ya kuteuliwa kwa mujbu w akura.

Akijibu hoja hizo Bakari amesema haoni haja ya kuw ana wasi wasi huo kwa kuwa suala hilo litaingizwa katika mapendekezo ya marekebisho ya katiba na baadae kuwasilishwa katika kikao cha baraza la wawakilishi jambo ambalo litawapa nafasi ya ya kutoa maoni yao juu ya uendeshaji wa suala hilo.

Hata hivyo suala la hoja ya makamu wa raias wa muungano Bakari alisema hakuna utata wowote kwa kuwa huyo atakuwa ni makamu wa rais wa Zanzibar kama vilivyo afasi nyengine za mawaziri wa Zanzibar.

Awali jana wawakilishi hao walionekana kuzungumza lugha laini tofauti ya siku ya kwanza katika kuchangia hoja binafsi iliyowasilishwa na kiongozi wa kambi ya upinzani Abubakar Kahmis Bakari.

Wakichangia hoja hiyo wajumbe mbali mbali kutoka CCM na CUF walionekana kutumia busara zaidi kuliko katika michango yao tofauti kabisa na siku ya mwanzo waipokuwa wakichangia hoja hiyo kwa kuwa zaidi upande wa CCM walionekana kusimamia hoja ya Butiama zaidi kuliko kukubaliana na hoja hiyo.

Ingawa baadhi ya wajumbe wao tokea kuanza mjadala huo walionekana kulainika mapema na kuwataka wenzao watumie hekima na busara zaidi katika michango kama walivyoelekezwa na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kuwataka kuwa makini zaidi na michago yao ili kujenga na kuepukana na jazba ambazo zimezoeleka katika vikao vya baraza hilo.

Mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Ramadhani Nyonje Pandu aliwahimiza wajumbe wenzake kuona umuhimu wa hoja hiyo na kuwataka waiunge mkono na kuacha kuvutana kwani hoja hiyo ikiwachwa itaweza kusababisha matatizo makubwa nchini.

"Napenda kwa mara ya kwanza nimsifu na kumpongeza maalim Seif kwa kukomaa kwake kisiasa na ukomavu wake wa kutaka mazungumzo ya kujenga umoja, mashirikiano na utulivu katika nchi yetu," alisema Pandu.

Mwenyekiti wa baraza la wawakilishi Ali Mzee Ali (CCM) naye aliunga mkono hoja na kuwataka wajumbe wenzake waungane kwani ni kitu kizuri kilichoanzishwa na ni muhimu sana kwa kuwaunganisha Wazanzibari ambao wamekuwa katika mazungumzo na hakuna haja yoyote ya kuikata hoja hiyo ambayo lengo lake ni kuwaunganisha Wazanzibari.

"Nakuombeni sana hoja hii tuipitishe kwa ..furaha na tusiwe na pingamizi hapana pahala mazuri kama hapa serikali ya shirikisho, umoja wa kitaifa ni mhimili mkuu katika nchi na Rais Karume yeye ndio kisiwa cha amani na utulivu jina lake Amani na anapenda amani na amani ndio hii tayari,"alisema.

Mwakilishi wa jimbo la Mkanyageni (CUF), Haji Faki Shaali alisema suala la kura ya maoni linatia hofu kutokana na historia kuwepo na shaka juu ya suala hilo kwa kuwa mara nyingi kura hizo huwa hazipigwi kwa haki na inavyotakiwa na ndio maana baadhi ya watu wengine huwa hawalitaki maana linaweza kusababisha mivutano kama ile ya uchaguzi ambayo mara huwagawa wananchi.

Mwakilishi aliyeteuliwa na rais, Juma Duni Haji (CUF) alisema haiwezekani kwa Wazanzibari kila baada ya miaka mitano kwanza wapigane na wauane ndio wapate rais kwanza jambo ambalo alisema wananchi wanapaswa kulikataa suala hilo kwani linaleta hasara kubwa katika jamii.

Alisema ni vizuri kutatarishwa kwa mazingira mazuri ili kuelekea uchaguzi mkuu na bila ya hivyo ni hatari kuingia katika uchaguzi kauli ambayo iliungwa mkono na waziri wa maji, ujenzi, nishati na ardhi, Mansoor Yussuf Himid ambaye kwa upande wake alisema hakuna haja ya kukimbilia uchaguzi wakati mazingira ni mabaya.

Mwakilishi wa Gando (CUF), Said Ali Mbarouk akichangia hoja hiyo alisema mawaziri wapatikane kwa kura na ukifanywa utaratibu wa wingi wa viti huenda vyama vidogo vikateketea na kupotea kabisa kwani chama kupata asilimia 10 ya kura za rais halafu kukiwacha nje haitakuwa vyema tutakuwa na vitakavyopata asilimia 5 na 10 na kupendekeza kwamba vile viti viwili vya upinzani wapewe wao maana wakiwekwa nje watakuwa ni waangalizi katika suala la demokrasia jambo ambalo sio zuri.

source mwananchi

0 comments:

Post a Comment