Manchester Yaizamisha Arsenal 3-1

Sunday, January 31, 2010 / Posted by ishak /


Manchester United imepunguza pengo la pointi kati yake na vinara wa ligi ya Uingereza, Chelsea kwa kuibanjua Arsenal magoli 3-1 kwenye uwanja wake wa Emirates.

Winga wa Manchester United toka Ureno, NANI ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Arsenal katika mechi ya leo.

Katika dakika ya 35, Nani baada ya kuwaramba chenga wachezaji watatu wa Arsenal alimimina majaro kati lakini kipa wa Arsenal, Manuel Almunia, aliusindika mpira huo kwenye nyavu zake katika harakati za kuuokoa.

Dakika nne baadae Nani tena alimpa pasi nzuri sana Wayne Rooney ambaye hakufanya ajizi kuiandikia Manchester goli la pili ambalo lilikuwa ni goli lake la 100 katika ligi ya Uingereza.

Mkorea Park Ji-Sung alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Arsenal kwenye dakika ya 52 baada ya kuambaa na mpira karibia nusu ya uwanja na kuachia shuti lililojaa kwenye ubavu wa kulia wa nyavu za Arsenal.

Wakati washabiki wa Arsenal wakianza kutoka uwanjani dakika 15 kabla ya mechi kuisha, Thomas Vermaelen aliipatia Arsenal goli la kufutia machozi kwenye dakika ya 80.

Akiongea baada ya kichapo hicho, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger aliwataka wachezaji wake kukusanya nguvu zao tena na kulipa kisasi kwa kuilaza Chelsea watakapokutana siku ya jumapili.


source nifahamishe