Jerry aumiza vichwa vya wabunge, wengi wahisi kasukiwa tuhuma

Thursday, February 04, 2010 / Posted by ishak /


Baadhi ya wabunge waliozungumza na NIFAHAMISHE walisema kuwa kitendo kilichofanywa na polisi dhidi ya Muro ni cha uonevu, huku wengine wakitaka sheria ichukue mkondo mara moja
Mbunge mmoja kwa tiketi ya CCM), aliyezungumza na NIFAHAMISHE aliyeomba kutotajwa jina alisema, suala la Muro kukamatwa kwa tuhuma za rushwa ni majungu kwani amekamatwa siku chache baada ya kuibua uovu unaofanywa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani aliowanasa wakipokea rushwa kutoka kwa madereva wa magari makubwa.

“Katika hali ya kawaida, hata mtu asiyejua sheria kutokana na maelezo yanayotolewa na jeshi la polisi dhidi ya Muro binafsi hayaeleweki kwani yanachanganya sana, hali inayoonyesha kwamba mashitaka ya mwanahabari huyo maarufu nchini aliyejipatia sifa kubwa kwa kufichua ufisadi nchini kwa sasa yamepikwa kumkomoa,” alisema mbunge huyo akionekena kukerwa na jambo hilo.

Amesema kama ni suala la rushwa hilo ni jambo la TAKUKURU wangeweka mitego yao na kumkamata na sio kama hivyo walivyopanga

“Inauma sana kuona mtu muhimu kama Jerry anatiwa mbaroni wakati amesaidia sana umma wa Tanzania hadi kupewa Tuzo ya Mwanahabari Bora kwa kuibua na kufichua mambo yaliyokuwa yakitendeka kwa kificho na hasa ndani ya Jeshi la Polisi na katika sekta nyingine muhimu nchini", alimalizia kusema mbunge huyo.

Kwa upande wa Mbunge maarufu anayewika nchini kwa kukosoa ufisadi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), alisema suala hili liangaliwe kwa undani ili kubaini ukweli uliojificha ndani yake.

Alisema ni vema ufanyike uchunguzi huru ambao hautaegemea upande wowote ili haki iweze kutendeka kwa kuwa watanzania wamekuwa hawataki kuambiwa ukweli.

Aidha, wabunge wengine waliotoa maoni yao walionyesha wasiwasi na kutaka kesi hiyo ipelekwe mahakamani mapema kama ilivyo kwa kesi nyingine badala ya kuendelea kuiweka mikononi mwa polisi kwa muda mrefu.

Hatahivyo jeshi la polisi nchini linasuasua kumfikisha mwanahabari huyo mahakamani kwa madai kuwa hadi wapate uthibitisho kutoka kwa wakili wa serikali.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment