Daktari wa nchini Slovenia aliyepigania mahakamani kwa miaka minne arudishiwe mbwa wake watatu ambao walikuwa wakiwang'ata watu, amefariki dunia baada ya kung'atwa na kujeruhiwa vibaya sana na mbwa hao.
Daktari huyo mwenye umri wa miaka 52 alipigania kwa miaka minne mahakamani kabla ya kushinda kesi na kurudishiwa mbwa wake ambao alinyang'anywa kutokana na matukio ya mbwa hao kuwang'ata watu.
Daktari huyo alikutwa jana akiwa amefariki kwenye bustani ya nyumba yake baada ya kung'atwa na kujeruhiwa vibaya na mbwa wake watatu aina ya "Bullmastiff".
Hadi polisi wanawasili kwenye nyumba yake katika mji mkuu wa Slovenia, Ljubljana, daktari huyo alikuwa ameishafariki lakini mbwa hao walikuwa wakiendelea kumshambulia.
Polisi walimpiga risasi na kumuua mbwa mmoja na kufanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi mbwa wengine wawili.
Mbwa hao walitumia muda mrefu sana kwenye jela za polisi wakati kesi hiyo iliyochukua miaka minne ikiendelea. Mbwa hao walitengwa na kuwekwa kwenye vyumba maalumu vyenye ulinzi mkali baada ya kumshambulia afisa aliyekuwa akiwahudumia.
Lakini baada ya kumalizika kwa hukumu iliyochukua masaa 11, mwezi juni mwaka jana, daktari huyo alishinda kesi na kukabidhiwa mbwa wake.
"Mbwa watatu wamemshambulia na kumuua mmiliki wao jana", alisema msemaji wa polisi Maja Adlesic.
Habari za kuuliwa kwa daktari huyo zimesababisha mjadala mkubwa nchini Slovenia huku chama cha upinzani kikimtaka waziri wa kilimo ajiuzulu kwa kushindwa kuzuia mbwa hao wasirejeshwe kwa mmiliki wao.
Polisi walikataa kutoa maelezo zaidi wala kulitaja jina la daktari huyo.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment