Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amekiri kuwasaliti wake zake watatu na kuzaa na mwanamke mwingine nje ya ndoa.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amezithibitisha taarifa za vyombo vya habari kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti wa rafiki yake na amemzalisha mtoto wa kike.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Zuma jana, Zuma amekiri kuwasaliti wake zake watatu na mchumba wake anayetegemea kumuoa hivi karibuni.
Mbali na kukiri uhusiano huo, rais Zuma amepinga vikali tuhuma kuwa anaonyesha mfano mbaya wakati harakati za kupambana na ukimwi zikiendelea nchini Afrika Kusini.
Asilimia 10 ya raia wa Afrika Kusini wanaishi na virusi vya ukimwi.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini viliripoti wiki hii kuwa Rais Zuma mwenye umri wa miaka 67 amezaa na binti wa rafiki yake wa karibu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kombe la dunia nchini Afrika Kusini.
Gazeti la Sunday Times la Afrika Kusini liliripoti kuwa Zuma alizisaliti ndoa zake na kuzaa na Sonono Khoza ambaye ni binti wa Irvin Khoza, mmiliki wa timu ya Orlando Pirates.
Sonono mwenye umri wa miaka 39 alijifungua mtoto wa rais Zuma mwezi oktoba mwaka jana.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, baba yake Sonono alielezea kuhuzunishwa sana na kitendo cha Zuma kumtia mimba binti yake.
Khoza aliiambia familia yake kuwa anahisi amesalitiwa na Zuma ambaye alikuwa akimchukulia kama rafiki yake wa karibu sana.
source nifahamishe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment