Daktari aliyebaka nje kwa dhamana

Wednesday, February 03, 2010 / Posted by ishak /

DAKTARI wa Hospital ya Marie Stopes tawi la Mwenge jijini Dar es Salaam, Paul Andrew (34), anayekabiliwa na tuhuma za kumbaka mgonjwa, amefikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana.
Daktari huyo ambaye ni mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu shtaka hilo la ubakaji mbele ya Hakimu Suzan Kihawa.

Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi, Nassor Sisiwayah, alidai mbele ya Hakimu huyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 26, mwaka huu, majira ya saa 7:00 mchana eneo Mwenge katika hospitali ya Marie Stopes.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa akiwa ni daktari wa hospitali hiyo, alitumia nafasi hiyo kumbaka mlalamikaji, Judith Keleth (30) bila idhini yake wakati akijitayarisha kumfanyia kipimo cha uchunguzi wa mimba cha Ultra Sound.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana shitaka hilo na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti aliyopewa.

Hakimu alimtaka Dokta Paul awe na wadhamini wawili ambao kila mmoja anatakiwa kusaini hundi la shilingi 500,000 kila mmoja.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 9 mwaka huu.


source nifahamishe